19 Machi 2011 - 20:30

Serikali ya Somalia imezitaka nchi za Afrika Mashariki kuisaidia katika kupambana na kundi la wanamgambo wa ash Shabab ambao wamehatarisha usalama wa nchi hiyo.

Taarifa ya serikali ya Somalia imetaka kutumwa vikosi vya Ethiopia nchini Somalia ili kukabiliana na kundi la wanamgambo wa ash Shabab. Wito huo umetolewa na serikali ya mpito ya Somalia katikla kikao cha Jumuiya ya Kieneo ya Nchi za Afrika Mashariki IGAD kinachoendelea katika mji mkuu wa Ethiopia Addis Ababa. Viongozi wa IGAD aidha wametangaza himaya na uungaji mkono wao kamili kwa Sheikh Sharif Sheikh Ahmed Rais wa serikali ya mpito ya Somalia.Wanamgambo wa ash Shabab wamekuwa wakiendesha vita dhidi ya serikali ya mpito ya Somalia hali ambayo imeifanya serikali hiyo kukabiliwa na changamoto kubwa ya kurejesha amani na usalama wa nchi. Hayo yanajiri huku watu wasiopungua 79 wakiripotiwa kuuawa katika mapigano makali kati ya wanamgambo wa kundi la ash Shabaab na wafuasi wa kundi lenye misimamo ya wastani lenye kuunga mkono serikali ya mpito ya Somalia la Ahlu Sunna Waljamaa katika eneo la Galguduud, katikati mwa nchi hiyo.